Serikali ya Uganda imeweka masharti mapya yanayotaka idhini ya maandishi kabla ya kuingizwa kwa vifaa vya huduma ya intaneti ya satelaiti ya Starlink, hatua inayokuja wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Januari.
Hatua hiyo imeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa watetezi wa haki za kidijitali na uhuru wa mawasiliano, wakihofia kuwa udhibiti huo unaweza kuwa njia ya kudhibiti mawasiliano na mtiririko wa taarifa wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Starlink, inayomilikiwa na kampuni ya SpaceX, inatoa huduma ya intaneti ya kasi ya juu kupitia satelaiti, na imekuwa ikitajwa kama suluhisho muhimu kwa miundombinu ya kidijitali barani Afrika, hususan katika maeneo yasiyofikiwa kirahisi na intaneti ya kawaida.
Hata hivyo, changamoto za kisheria na udhibiti wa serikali zimeendelea kuikwamisha Starlink katika mataifa kadhaa ya Afrika, huku baadhi ya serikali zikionyesha tahadhari juu ya athari zake katika usalama wa taifa na udhibiti wa mawasiliano.
Hatua ya Uganda sasa inaongeza mjadala mpana kuhusu uwiano kati ya usalama wa taifa, uhuru wa mtandao, na demokrasia katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
Chanzo; Cnn