Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara ameshinda uchaguzi wa urais kwa mara ya nne mfululizo baada ya kupata asilimia 89.77 ya kura, kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa jana na Tume Huru ya Uchaguzi (CEI).
Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi, takriban wananchi milioni tisa walistahili kupiga kura, huku wagombea wakuu wa upinzani wakitengwa katika kinyang’anyiro hicho.
Rais wa zamani Laurent Gbagbo alizuiwa kugombea kutokana na hukumu ya jinai, wakati aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Credit Suisse, Tidjane Thiam, alinyimwa fursa hiyo kutokana na kuwa na uraia wa Ufaransa.
Wagombea waliobaki wanne hawakuwa na nguvu kubwa kisiasa kutokana na kukosekana rasilimali za kifedha.
Miongoni mwao, aliyekuwa Waziri wa Biashara, Jean-Louis Billon, aliyempongeza Ouattara mapema Jumapili, alipata asilimia 3.09, huku Simone Gbagbo, akipata asilimia 2.42 ya kura.
Mwenyekiti wa CEI, Ibrahime Coulibaly-Kuibiert, amesema idadi ya wapigakura ilikuwa takriban asilimia 50, kiwango kinachofanana na chaguzi za urais za mwaka 2010 na 2015, lakini chini ya asilimia 80 ya wapigakura waliojitokeza katika awamu ya kwanza ya mwaka 2010.
Akinukuliwa na kituo cha Al Jazeera, mwandishi Ahmed Idris amesema ushindi huo wa Ouattara umetokana na kutokuwepo wapinzani wakuu na mwitikio mdogo wa wapigakura.
Chanzo: Mwananchi