Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeitaka Benki ya Dunia kuishinikiza serikali ya Uganda kuifuta sheria kali dhidi ya watu wanashiriki mapenzi ya jinsia moja kabla ya kurejeshwa tena kwa ufadhili uliokuwa umesitishwa.
Wito wa Amnesty umetolewa baada ya afisa mmoja wa wizara ya fedha nchini Uganda kusema mapema wiki hii kwamba nchi hiyo itapokea kwa muda wa miaka mitatu jumla ya dola bilioni 2 kutoka kwa Benki ya Dunia ambayo ilisitisha mikopo yote kwa Uganda baada ya rais Yoweri Musevi kusaini mwaka 2023 sheria hiyo dhidi ya jamii ya LGBTQ+.
Wakati huo Benki ya Dunia ilisema kuwa miradi yote inayoifadhili inapaswa kuzingatia sera zake zisizo za kibaguzi. Sheria ya Uganda dhidi ya ushoga ni mojawapo ya sheria kali zaidi duniani ikijumuisha wakati mwengine hukumu ya kifo katika baadhi ya matukio.
Chanzo: Dw