Ajali ya basi la abiria imesababisha vifo vya watu wasiopungua 16 katika kisiwa kikuu cha Java, nchini Indonesia, baada ya basi hilo kupata ajali mbaya muda mfupi baada ya saa sita usiku wa kuamkia Jumatatu, kwa mujibu wa maafisa wa usalama na uokoaji.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka husika, basi hilo lilikuwa likisafirisha abiria 34 likitokea mji mkuu Jakarta kuelekea Yogyakarta. Ajali ilitokea wakati basi hilo likipanda barabara ya kulipia ushuru (toll road) na kujaribu kuingia katika njia ya kutokea, ambapo lilipoteza mwelekeo na kupata ajali.
Maafisa wa uokoaji wamesema kuwa juhudi za kuokoa manusura ziliendelea mara baada ya tukio hilo, huku waliojeruhiwa wakikimbizwa katika hospitali za karibu kwa ajili ya matibabu. Uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea kufanywa na mamlaka za usalama barabarani nchini humo.
Chanzo; Bongo 5