Kiongozi wa Upinzani Nchini Venezuela, Maria Corina Machado, ametunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu kwa juhudi zake katika kutetea haki za kidemokrasia na kupigania mabadiliko ya kisiasa Nchini humo.
Machado ambaye ana umri wa miaka 58 mwenye taalum ya Uhandisi wa Viwanda, ameishi mafichoni tangu mwaka 2024 baada ya Mahakama za Venezuela kumzuia kugombea Urais ambapo uamuzi huo ulimnyima nafasi ya kumkabili Rais Nicolas Maduro ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2013.
Tuzo ya mwaka huu imekuja huku ikitawaliwa na mjadala kuhusu kauli za mara kwa mara za Rais wa Marekani Donald Trump, aliyedai anastahili tuzo hiyo kutokana na juhudi zake za kupendekeza mpango wa kusitisha vita Gaza lakini Wachambuzi wa masuala ya Nobel wameeleza kabla ya tangazo hilo kuwa Trump alikuwa na uwezekano mdogo kushinda kutokana na sera zake zinazodaiwa kudhoofisha utaratibu wa Kimataifa ambao kamati ya Nobel inauenzi.
Tuzo ya Amani ya Nobel yenye thamani ya Kronor milioni 11 za Uswidi (sawa na takribani dola milioni 1.2 za Marekani) itakabidhiwa rasmi Jijini Oslo, Norway, tarehe 10 Desemba, siku ya kumbukumbu ya kifo cha Alfred Nobel, mwanzilishi wa tuzo hizo mwaka 1895.
Chanzo: Millard Ayo