Helikopta ya Jeshi la Wanamaji la Marekani aina ya MH-60R Seahawk na ndege ya kivita aina ya F/A-18F Super Hornet zimepata ajali ndani ya nusu saa, wakati wa shughuli za kawaida za mazoezi juu ya Bahari ya Kusini ya China, kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Wanamaji la Marekani (Pacific Fleet).
Wafanyakazi wote waliokuwa ndani ya ndege hizo wameokolewa wakiwa salama. Jeshi la Wanamaji limeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hizo mbili zilizotokea karibu na meli ya kubebea ndege ya USS Nimitz. Rais Donald Trump amezitaja ajali hizo kama “zisizo za kawaida,” na ameashiria uwezekano wa tatizo la mafuta kuwa chanzo.
Ajali hizi zimetokea wakati Marekani ikiendelea kuimarisha uwepo wake katika Bahari ya Kusini ya China eneo lenye mvutano mkubwa wa madai ya umiliki kati ya mataifa kadhaa ya Asia ya Kusini Mashariki, huku China ikidai sehemu kubwa ya bahari hiyo kinyume na uamuzi wa mahakama ya kimataifa. Marekani imekuwa ikisisitiza uhuru wa meli kupita na biashara huru katika eneo hilo.
Nimitz, mojawapo ya meli kubwa na kongwe zaidi za kubebea ndege za kivita za Marekani, inatarajiwa kustaafishwa mwaka ujao.
Jeshi la Wanamaji la Marekani limepoteza ndege nne aina ya F/A-18 mwaka huu pekee, ikiwemo mbili zilizopata ajali katika Bahari Nyekundu na nyingine iliyopata matatizo wakati wa mazoezi huko Virginia. Ajali hizi zinatokea wakati Rais Trump yuko katika ziara ya kidiplomasia barani Asia, ambapo anatarajiwa kukutana na Rais wa China Xi Jinping kwa mazungumzo kuhusu biashara, kufuatia kupungua kwa mvutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Chanzo: Global Publishers