Tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha 7.4 limepiga eneo la kusini mwa Ufilipino leo Ijumaa, huku maonyo ya tsunami yakitolewa katika nchi kadhaa na watu katika maeneo ya pwani ya karibu wakihimizwa kuhamia bara au kwenye ardhi ya juu.
Shirika la Phivolcs limetahadharisha kuhusu mitetemeko ya baada ya tetemeko hilo, ambalo lilitokea asubuhi kwenye maji karibu na mji wa Manay huko Davao Oriental katika eneo la Mindanao. Mtu mmoja ameuawa, kwa mujibu wa afisa wa ulinzi wa raia Raffy Alejandro kwenye mtandao wa Facebook.
Kituo cha Maonyo yaTsunami cha Pasifiki kumetoa chapisho majira ya saa sita mchana kwa saa za huko kikisema tishio la tsunami nchini Ufilipino lilikuwa limepita, baada ya kusema mapema mawimbi ya urefu wa mita 1 hadi 3 yanawezekana, ingawa kulisalia maonyo kutoka kwa mashirika mengine.
Hakukuwa na ripoti zingine za majeruhi kutoka ofisi za maafa katika eneo hilo lakini afisa mmoja huko Manay amesema kulikuwa na ripoti za awali za uharibifu wa nyumba, majengo na madaraja.
Tetemeko hilo lilikuwa kati ya matetemeko makubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni kuikumba Ufilipino, ambayo iko kwenye “Ring of Fire" ya Pasifiki na kukumbwa na matetemeko zaidi ya 800 kila mwaka.
Chanzo: East Africa Radio