Serikali ya Rwanda imefunga zaidi ya makanisa 10,000 baada ya kubainika kushindwa kutimiza masharti ya sheria ya mwaka 2018 inayodhibiti uendeshaji wa maeneo ya ibada nchini humo.
Sheria hiyo iliweka masharti mapya yanayohusu afya na usalama wa waumini pamoja na uwazi wa kifedha, sambamba na hitaji la kila mhubiri kuwa na mafunzo ya theolojia kabla ya kuongoza ibada.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amesema haoni mchango wa maana wa baadhi ya makanisa katika kutatua changamoto kubwa zinazoikabili dunia, ikiwemo vita na ukosefu wa ajira.
Rais Kagame amebainisha kuwa badala ya kusaidia jamii, baadhi ya makanisa yanatumika kama njia ya kujinufaisha binafsi kwa viongozi wake, hali iliyochangia Serikali kuchukua hatua za kisheria ili kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha maeneo ya ibada yanaendeshwa kwa misingi inayokubalika kisheria.
Chanzo; Nipashe