Nchini Ujerumani, idadi ya Wakristo inapungua kwa kiasi kikubwa. Matokeo yake ni makanisa mengi kubaki bila kutumiwa. Kwa mara ya mwisho, Kanisa la Mtakatifu Anna (St. Anna) limejaa karibu waumini wote.
Kwaya inaimba, na kinanda kidogo kinatoa hamasa wakati wa uimbaji. Lakini hii ni Misa ya mwisho kabisa katika kanisa dogo la Kikatoliki la Gildehaus, eneo la Bad Bentheim karibu na mpaka wa Ujerumani na Uholanzi. Kuanzia sasa, jengo hili halitakuwa tena nyumba ya ibada.
Kuelekea mwisho wa ibada, kufungwa kwa kanisa hili kunakuwa halisi kabisa. Waumini kutoka katika parokia wanafungua madhabahu na kutoa masalia ya watakatifu (reliquia).
Hivi ni vitu vidogo vinavyomwakilisha mtakatifu, kama vipande vya mifupa au vitambaa, ambavyo kwa kawaida huwekwa ndani ya madhabahu ya kanisa la Kikatoliki lililowekwa wakfu.
Idadi ya wanachama wa makanisa nchini Ujerumani inapungua kwa kasi kubwa. Mwaka 2024 pekee, makanisa mawili makubwa yalipoteza zaidi ya Wakristo milioni moja kutokana na watu kujiondoa kanisani na vifo.
Kwa sasa, ni takribani asilimia 45 tu ya Wajerumani wanaoendelea kuwa wanachama wa Kanisa la Kiinjili la Ujerumani (EKD) au Kanisa Katoliki. Miaka 30 iliyopita, idadi hiyo ilikuwa karibu asilimia 69.
Chanzo; Nipashe