Mahakama nchini Mali imemhukumu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Moussa Mara, kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kuchapisha ujumbe wa mtandaoni uliodaiwa kukosoa mamlaka ya serikali na kuunga mkono wapinzani wa kisiasa walioko gerezani.
Mara (50), ambaye aliwahi kuongoza serikali ya Mali kwa miezi minane kipindi cha mwaka 2014 hadi 2015, alihukumiwa jana Jumatatu na Mahakama ya Kituo cha Kitaifa cha Makosa ya Mtandao mjini Bamako.
Pamoja na kifungo hicho cha mwaka mmoja jela, mahakama pia ilimpa adhabu ya kifungo cha miezi 12 pamoja na faini ya faranga za CFA 500,000 (sawa na takriban Sh1.5 milioni).
Mara amekuwa gerezani tangu Agosti 1, wiki chache baada ya kuchapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii X (zamani Twitter), akiwataja baadhi ya wafungwa wa kisiasa aliowatembelea na kueleza msimamo wake.
Katika ujumbe huo wa Julai 4, Mara aliandika: “Kadri usiku unavyodumu, jua litaonekana! Tutapambana kwa njia zote ili hilo litokee haraka iwezekanavyo.”
Hukumu hiyo imekuja wakati serikali ya kijeshi ya Mali, ambayo ilichukua madaraka kupitia mapinduzi mwaka 2021, ikiendelea kukosolewa kwa kukandamiza uhuru wa maoni na kuwakamata viongozi wa kisiasa wanaoonyesha upinzani.
Chanzo: Mwananchi