Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Trump Azipiga Marufuku BBC, Politico Kuripoti Ikulu ya Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa anazipiga marufuku “mara moja” CNN, MS NOW na Politico kuingia Ikulu ya White House, hatua ya hivi karibuni katika uhusiano wake wenye mvutano na vyombo vya habari.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social siku ya Ijumaa, Trump alisema vyombo hivyo vya habari “vinaandika au kuripoti hadithi za kubuni na uongo mara kwa mara” kuhusu utawala wake, ingawa hakutoa mifano maalum ya madai hayo.

Baadaye, Trump aliita hatua hiyo kuwa “marufuku rahisi sana”, lakini hakufafanua jinsi itakavyotekelezwa. Bado haijulikani ikiwa wafanyakazi wa vyombo hivyo watazuiwa kuingia katika eneo la White House.

CNN ilikosoa haraka uamuzi huo, ikiutaja kuwa “shambulio haramu” dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Marekani. Hatua hiyo inatarajiwa kukabiliwa na changamoto za kisheria.

Waandishi wa Politico na CNN walionekana wakiwa bado ndani ya eneo la White House muda mfupi baada ya tangazo hilo kutolewa. Wakati huo huo, kikosi cha CNN kilikuwa kikisafiri pamoja na Makamu wa Rais JD Vance kwenda na kurudi kutoka tukio lililofanyika Iowa.

Katika taarifa yake, CNN ilisema marufuku hiyo, ikiwa itatekelezwa, ni kinyume cha sheria na ikaeleza kuwa inaunga mkono kikamilifu timu yake ya White House pamoja na taarifa wanazotoa kwa usahihi na kwa haki.

“Tuna haki chini ya Katiba ya Marekani kufanya kazi hiyo ya uandishi wa habari bila kuzuiwa au kuingiliwa na serikali,” ilisema CNN. “Iwapo marufuku ambayo Rais Trump ameihusisha itatekelezwa, itakuwa shambulio haramu dhidi ya haki hiyo ya msingi inayolindwa na Katiba.”

Politico nayo ilitoa taarifa ikisema itaendelea kuripoti kwa haki kuhusu White House ya sasa na zile zijazo.

“Tutalinda kwa nguvu zote haki zetu chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba dhidi ya jaribio lolote la kuzizuia,” ilisema Politico.

MS NOW, ambayo zamani ilijulikana kama MSNBC, ilikataa kutoa maoni.

Katika ujumbe wake, Trump alisema: “Vyombo vya habari havipaswi kuruhusiwa kuandika au kuripoti hadithi za kubuni na uongo kila mara vinaporipoti kuhusu Rais wa Marekani, utawala wa Trump au Marekani. Vyombo vingine vya habari vitafuata.”

Ujumbe huo haukutaja taarifa au habari maalum zilizochochea hatua hiyo.

Alipoulizwa na mwandishi wa habari kuhusu kauli yake ya kusema “vyombo vingine vitafuata”, Trump alijibu: “Kama unamaanisha habari za uongo? Unajua, The New York Times ni habari za uongo, Washington Post ni habari za uongo.”

Rais wa Chama cha Waandishi wa White House (WHCA), Jacqui Heinrich, alisema chama hicho kinasimama kuwatetea waandishi wa habari wanaolengwa kwa kufanya kazi zao.

“Hili ni suala kubwa zaidi ya haki za waandishi wa habari,” alisema Heinrich, ambaye pia anafanya kazi Fox News. “Ni kuhusu haki ya wananchi wa Marekani kupata taarifa kamili na huru kuhusu shughuli, sera na maamuzi ya mtu yeyote anayeshikilia ofisi ya juu zaidi nchini.”

Baadaye akiwa katika Ofisi ya Oval, Trump alisema hakukuwa na sababu maalum ya kutangaza hatua hiyo Ijumaa alasiri.

“Ni mkusanyiko wa habari mbalimbali za miaka ya hivi karibuni. Unachoka nazo,” alisema.

Aliongeza kuwa “huenda vyombo vingine vikajiunga na orodha hiyo,” lakini hakuvitaja.

Trump pia alikiri kuwa hatua hiyo inaweza kupingwa mahakamani, akisema: “Nafikiri ni vizuri kuonyesha jambo hili, iwe litaendelea au halitaendelea.”

Tangu arejee madarakani Januari 2025, Trump na maafisa wa utawala wake wamekuwa wakikwaruzana mara kwa mara na waandishi wa habari wa White House. Katika muhula wake wa pili, Trump pia amefungua nafasi kwa wanablogu wa kihafidhina, washawishi wa mitandaoni (influencers) na vyombo vingine vya habari kuingia katika chumba cha waandishi wa habari, akisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mitazamo tofauti inawafikia Wamarekani.

Mwezi Februari, White House ilitangaza kuwa inachukua udhibiti wa kundi la waandishi wa habari (press pool) linalopata fursa ya kumfuatilia Trump, jukumu ambalo kwa zaidi ya karne moja lilikuwa likisimamiwa na Chama cha Waandishi wa White House.

Katika mwezi huo huo, utawala wa Trump ulizuia waandishi na wapiga picha wa Associated Press (AP) kuingia katika maeneo yenye ufikiaji maalum kama Ofisi ya Oval na ndege ya Air Force One, kwa sababu shirika hilo liliendelea kutumia jina “Gulf of Mexico” badala ya “Gulf of America”.

AP iliwasilisha kesi mahakamani mara moja na mchakato huo bado unaendelea.

Trump amekuwa akigongana mara kwa mara na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval, ndani ya Air Force One na katika matukio ya White House, mara nyingi akiwaita “habari za uongo” na “wasio na adabu”.

Katika muhula wake wa kwanza wa urais, Trump pia alimzuia mwandishi wa CNN Jim Acosta kuingia White House, lakini baadaye alirejeshewa kibali chake baada ya CNN kufungua kesi mahakamani.

CNN ni mojawapo ya vyombo vitano pekee vya habari nchini Marekani vinavyorekodi video kwa ajili ya press pool. Mfumo huo unahusisha chombo au mwandishi mmoja kushiriki taarifa na picha za matukio ya rais na vyombo vingine vya habari. BBC nayo ni sehemu ya kundi la redio la White House.

Tangazo hilo lilikosolewa mara moja na mashirika mbalimbali yanayotetea uhuru wa vyombo vya habari.

Taasisi ya Knight First Amendment katika Chuo Kikuu cha Columbia ilisema kuwa, kutokana na mahakama nyingi tayari kutoa maamuzi dhidi ya Trump katika masuala kama hayo, ilitarajiwa angekuwa amejifunza.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Jameel Jaffer, alisema kuwa ikiwa Trump atakusudia kuviondoa vyombo hivyo katika press pool ya White House, hatua hiyo itakuwa kinyume cha Katiba kwa sababu press pool ni “jukwaa la umma” chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba.

Kamati ya Waandishi wa Habari kwa Ajili ya Uhuru wa Vyombo vya Habari (Reporters Committee for Freedom of the Press), ambayo hutoa huduma za kisheria kwa vyombo vya habari, ilisema inatarajia marufuku hiyo kufutwa haraka mahakamani kwa kuwa “ni kinyume cha Katiba kwa uwazi kabisa”.

“Marekebisho ya Kwanza yanaeleza wazi kuwa White House ikisharuhusu baadhi ya waandishi wa habari, haiwezi kuwazuia wengine kwa sababu haipendi wanavyoripoti,” alisema rais wa kundi hilo, Bruce Brown, akitaja hatua hiyo kuwa “ubaguzi wa mitazamo”.

Freedom of the Press Foundation nayo ilisema marufuku hiyo ni kinyume cha sheria na kuongeza: “Ni vigumu pia kufikiria hatua nyingine isiyo na busara zaidi ya hii.”

Shirika hilo lilisema Trump amekuwa akijibu kwa kulipiza kisasi dhidi ya vyombo vya habari kwa miaka mingi, lakini hatua hizo hazijamsaidia, likiongeza kuwa “mashambulizi haya makubwa yanaonyesha jinsi anavyohofia wananchi wenye taarifa sahihi”.

Trump amechukua hatua za kisheria dhidi ya vyombo mbalimbali vya habari vya Marekani na kimataifa, vikiwemo The Wall Street Journal, The New York Times na BBC.

Kuhusiana na mada hii: