Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Taiwan dhidi ya kutangaza rasmi uhuru kutoka China.
“Sina nia ya kuona mtu yeyote akitangaza uhuru,” rais huyo wa Marekani aliliambia Fox News siku ya Ijumaa, mwishoni mwa mkutano wake wa siku mbili na rais wa China Xi Jinping mjini Beijing.
Rais wa Taiwan Lai Ching-te awali alisema kuwa Taiwan haina haja ya kutangaza rasmi uhuru kwa sababu tayari inajiona kama taifa huru lenye mamlaka yake.
Kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikiunga mkono Taiwan, ikiwa ni pamoja na kuwajibika kisheria kuipatia uwezo wa kujilinda, lakini mara nyingi imekuwa ikijikuta ikihitaji kusawazisha uhusiano huo na diplomasia yake na China.
Trump awali alisema kuwa “hakutoa ahadi yoyote upande wowote” kuhusu kisiwa hicho kinachojitawala ambacho China inadai kuwa sehemu ya eneo lake, huku ikiwa haijaondoa uwezekano wa kukichukua kwa nguvu.
Msimamo rasmi wa Washington ni kwamba haiungi mkono uhuru wa Taiwan, huku uhusiano wake na Beijing ukiendelea kwa masharti ya kukubali kuwa kuna serikali moja tu ya China.
Beijing imekuwa ikionyesha wazi kutofurahishwa na rais wa Taiwan, ambaye awali ilimuita “msumbufu” na “mharibifu wa amani ya pande mbili za mlango wa Taiwan”.
Wananchi wengi wa Taiwan wanajiona kuwa sehemu ya taifa tofauti, ingawa wengi wao wanaunga mkono kuendelea kwa hali ya sasa ambapo Taiwan haitangazi uhuru kutoka China wala kuungana nayo.
Katika mahojiano yake na Fox News, Trump alisisitiza kuwa sera ya Marekani kuhusu suala hilo haijabadilika.
“Unajua, tunatarajiwa kusafiri maili 9,500 kupigana vita. Sitafuti hilo. Nataka watulie. Nataka China itulie,” alisema.
Akiwa kwenye safari ya kurejea Washington, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye na Xi walizungumza “mara nyingi” kuhusu Taiwan, lakini alikataa kujibu iwapo Marekani ingeilinda kijeshi.
Trump alisema Xi “ana hisia kali sana” kuhusu Taiwan na “hataki kuona harakati za uhuru”.
“Kwenye mahusiano ya China na Marekani, suala la Taiwan ndilo muhimu zaidi,” Xi alionya wakati wa mazungumzo hayo, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya China, akiongeza kuwa: “Likishughulikiwa vibaya, mataifa haya mawili yanaweza kugongana au hata kuingia kwenye mzozo.”
Alipoulizwa kama anaona uwezekano wa mgogoro kati ya China na Marekani kuhusu Taiwan, Trump alisema: “Hapana, sidhani hivyo. Nafikiri mambo yatakuwa sawa. Xi hataki kuona vita.”
China imeongeza mazoezi ya kijeshi karibu na kisiwa hicho katika miaka ya hivi karibuni, jambo lililoongeza mvutano katika eneo hilo na kujaribu mizani ambayo Washington imekuwa ikiidumisha.
Mwishoni mwa mwaka jana, utawala wa Trump ulitangaza mpango wa kuuza silaha wenye thamani ya dola bilioni 11 kwa Taiwan, ukiwemo mfumo wa kisasa wa kurusha makombora na aina mbalimbali za makombora, jambo ambalo Beijing ililikosoa vikali.
Trump alisema hivi karibuni ataamua kama mauzo hayo yataendelea, akiongeza kuwa yeye na Xi walijadili suala hilo “kwa kina sana”.
Aliongeza: “Nitazungumza na mtu ambaye kwa sasa, mnajua ni nani huyo, anaiongoza Taiwan.”
Marekani haina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Taiwan, ingawa inaendelea kuwa na uhusiano mkubwa usio rasmi. Kwa kawaida marais wa Marekani hawazungumzi moja kwa moja na rais wa Taiwan, kwani kufanya hivyo kunaweza kuongeza mvutano mkubwa na Beijing, ambayo inamchukulia Lai Ching-te kama mtenganishaji.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Taiwan Chen Ming-chi alisema Jumamosi kuwa Taiwan itahitaji kufafanua maana halisi ya kauli za Trump.
Chen pia alisema kuwa mauzo ya silaha za Marekani kwa Taiwan yameidhinishwa chini ya sheria za Marekani.
“Mauzo ya silaha kati ya Taiwan na Marekani yamekuwa msingi wa amani na uthabiti wa kikanda,” alisema.
Msemaji wa Rais Lai, aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters, alisema mauzo ya silaha ya Marekani ni sehemu ya “ahadi ya usalama ya Marekani” kwa Taiwan na “yanatumika kama njia ya pamoja ya kuzuia vitisho vya kikanda”.
Trump pia aliiambia Fox News: “Hatutafuti vita, na kama hali itaendelea kama ilivyo, nafikiri China itaridhika na hilo. Lakini hatutaki mtu yeyote kusema, ‘Twende tukatangaze uhuru kwa sababu Marekani inatuunga mkono.’”
Marekani hapo awali iliwahi kuikasirisha China kwa kuonekana kulegeza msimamo wake kuhusu uhuru wa Taiwan.
Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliondoa tamko kutoka kwenye tovuti yake lililosisitiza upinzani wa Washington dhidi ya uhuru wa Taiwan mwezi Februari 2025, jambo ambalo Beijing ilisema “linatoa ishara mbaya kwa makundi ya wanaotaka kujitenga”.
Maafisa wa Marekani nchini Taiwan wakati huo walisema: “Kwa muda mrefu tumekuwa tukipinga mabadiliko yoyote ya upande mmoja kwenye hali ilivyo kutoka upande wowote.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Taiwan Lin Chia-lung alisema timu yake ilikuwa ikifuatilia mkutano wa Marekani na China na imeendelea kuwa na mawasiliano mazuri na Marekani pamoja na mataifa mengine “ili kuhakikisha kuimarika kwa uhusiano wa Taiwan na Marekani na kulinda maslahi ya Taiwan”.
Alisema Taiwan imekuwa “mlinzi wa amani na uthabiti” katika eneo hilo na akaishutumu China kwa kuongeza hatari kupitia “hatua zake za kijeshi za uchokozi na ukandamizaji wa kimabavu”.