Burudani na maonesho ya tamaduni kutoka mataifa mbalimbali duniani zimetawala katika hafla ya ufunguzi wa Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026 linalofanyika jijini Ekaterinburg nchini Urusi.

Kabla ya kuanza rasmi kwa tamasha hilo, wawakilishi kutoka mabara mbalimbali walipata fursa ya kuonesha utamaduni wa nchi zao kupitia mavazi ya asili, muziki na ngoma zilizobeba utambulisho wa mataifa yao, hali iliyozua msisimko mkubwa miongoni mwa washiriki.
Maelfu ya vijana kutoka nchi mbalimbali duniani walihudhuria hafla hiyo iliyolenga kuunganisha vijana kupitia majadiliano, ubunifu, utamaduni na ushirikiano wa kimataifa.

Katika ufunguzi huo, washiriki walipokea salamu maalum kutoka kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, aliyewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kujenga mustakabali wao na kuchangia maendeleo ya jamii zao.

Putin alisema Urusi ni nchi inayotoa nafasi kwa vijana kutimiza ndoto zao kupitia elimu, ubunifu, sayansi na teknolojia, huku akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa vijana katika kujenga dunia ya kesho.
Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026 limewakutanisha maelfu ya washiriki kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha urafiki, kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya vijana duniani.