Rais wa Marekani, Donald Trump amesema inapaswa ashiriki katika mchakato wa kumchagua kiongozi mkuu ajaye wa Iran, akisisitiza kuwa anatamani kuona uongozi mpya ambao utakuwa na mahusiano mazuri na Marekani.
Kauli hiyo imekuja wakati wa mvutano wa kijeshi kati ya pande hizo, huku Trump akisema pia hapendi kuona kiongozi mkali akichukua madaraka kwa sababu hali hiyo inaweza kuisukuma Marekani kurejea vitani na Iran katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Katika ujumbe wa video aliouchapisha baada ya kuanza kwa operesheni ya kijeshi aliyoitaja kama “Operation Epic Fury,” Trump aliwahimiza wananchi wa Iran kuchukua udhibiti wa serikali yao baada ya operesheni hiyo kukamilika.
Aidha, ameripotiwa kupinga wazo la Mojtaba Khamenei kuchukua nafasi ya baba yake, Ali Khamenei, akisema Marekani ina maslahi ya kuona uongozi mpya unaoleta mabadiliko katika mfumo wa utawala wa Iran.
Trump pia amesema angeona ni jambo “zuri” iwapo vikosi vya Wakurdi wa Iran vilivyopo nchini Iraq vingeingia Iran kushambulia majeshi ya usalama ya nchi hiyo. Hata hivyo, amesema hana wasiwasi kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta nchini Marekani kutokana na mgogoro huo, akisisitiza kuwa operesheni ya kijeshi ya Marekani ndiyo kipaumbele chake kikuu kwa sasa.
Chanzo; Eatv