Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema taifa lake halitapiga magoti mbele ya shinikizo la Marekani na Israel licha ya vita vilivyodumu kwa karibu miezi saba, huku akisisitiza kuwa Tehran iko tayari kwa mazungumzo ya kidiplomasia endapo maslahi yake yatazingatiwa.
Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Pezeshkian alijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump aliyetoa onyo la kuiangamiza Iran ikiwa makubaliano mapya hayatapatikana kwa haraka.
"Upinzani wa wananchi wa Iran utaongezeka kadri vikwazo, mashinikizo na vitisho vinavyoongezeka. Hatutainamisha vichwa vyetu wala kupiga magoti," alisema.
Rais huyo alisema makubaliano yoyote kati ya Tehran na Washington lazima yajumuishe kuondolewa kwa mzingiro wa Marekani dhidi ya meli na bandari za Iran pamoja na kurejeshwa kwa uhuru wa usafiri wa majini katika Mlango Bahari wa Hormuz.
"Haiwezekani mataifa mengine yote yanufaike na njia hiyo muhimu ya bahari huku Iran ikinyimwa haki ya kuitumia," alisema.
Hotuba ya Pezeshkian ilifanyika wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka kufuatia vita vilivyoanza mwishoni mwa Februari baada ya mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya malengo ya Iran.
Katika hotuba yake, rais huyo aliishutumu Marekani kwa kile alichokiita sera za mabavu na kuonyesha picha ya Kiongozi Mkuu wa zamani wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ambaye aliuawa katika shambulio lililolenga makazi yake wakati wa operesheni hiyo ya kijeshi.
Pezeshkian pia aliwasilisha picha za baadhi ya raia zaidi ya 175 ambao Iran inadai waliuawa katika mashambulizi yaliyolenga shule ya msingi mjini Minab na kituo cha michezo mjini Lamerd. Marekani imekanusha kuhusika na shambulio la Lamerd na kusema bado inachunguza kilichotokea Minab.
"Wananchi wetu wasio na hatia wamekuwa walengwa wa mashambulizi ya kikatili dhidi ya nchi yetu, lakini tulijilinda kwa nguvu zote," alisema.
Wakati huo huo, shambulio dhidi ya meli ya mizigo katika Mlango Bahari wa Hormuz limeripotiwa kumuua baharia mmoja raia wa India, hatua iliyozua wito mpya wa kurejeshwa kwa usalama wa usafiri katika njia hiyo muhimu inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi inayosafirishwa duniani.
Mwezi Juni, Marekani na Iran zilifikia makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano na kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, lakini makubaliano hayo yalivunjika baada ya mashambulizi dhidi ya meli kuanza tena na Marekani kurejesha mzingiro wake.
Licha ya msimamo wake mkali, Pezeshkian alisema Iran bado inaamini katika diplomasia.
"Tuko tayari kwa mazungumzo na majadiliano, lakini hatutakubali lugha ya vitisho au matumizi ya nguvu," alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa Iran haitaachana na mpango wake wa nyuklia kwa matumizi ya amani huku akikanusha madai kuwa taifa hilo lina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia.
Kauli hiyo imekuja wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja chini ya usimamizi wa Qatar pembeni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, Tehran imeendelea kusisitiza kuwa kuondolewa kwa mzingiro wa Marekani na kuachiwa kwa mali za Iran zilizogandishwa nje ya nchi ni miongoni mwa masharti muhimu kabla ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote mapya.