Taasisi ya sanaa ya Kitanzania, Rangi Gallery, imeandika historia kwa kuwa ya kwanza kutoka nchini kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya Art OnO yaliyofanyika jijini Seoul, Korea Kusini. Maonesho hayo yanatajwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa na yenye upekee katika sekta ya sanaa barani Asia.
Maonesho ya Art OnO—yenye maana ya *Art One and Only*—yalifanyika kwa mara ya tatu katika kituo cha SETEC, yakihusisha washiriki 35 kutoka nchi 12, ikiwemo Japan, Ujerumani na Uswisi.
Katika tukio hilo, Rangi Gallery iliwasilisha kazi za wasanii wanne wanawake kutoka Tanzania ambao ni Theresia Venance, Tulsi Patel, Valerie Asiimwe Amani na Turakella Editha Gyindo. Kila mmoja aliwasilisha kazi zilizobeba taswira ya utamaduni, mila na maisha ya Kitanzania.
Theresia Venance aliwasilisha michoro ya maumbo ya binadamu yenye kuonyesha nguvu ya mwanamke, huku Valerie Asiimwe Amani akiwasilisha kazi zinazoakisi tamaduni mbalimbali duniani. Kwa upande wake, Tulsi Patel alitumia dhana ya maji na mtiririko wake kuwasilisha taswira ya kina ya mwili wa binadamu.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Rangi Gallery, Lorna Mashiba Albou, alisema kuwa ingawa wasanii wote waliowasilishwa walikuwa wanawake, hilo halikupangwa mahsusi bali lilitokana na ubora wa kazi zao.
“Wanawake hawa wanne wameiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa hili la kimataifa, jambo linaloonesha kukua kwa vipaji vya wasanii wanawake na kutambulika kwake duniani,” alisema.
Rangi Gallery ilianzishwa jijini Dar es Salaam na Lorna Mashiba Albou, ambaye awali alifanya kazi kama mwanasheria kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya kujikita katika sanaa ya ubunifu. Taasisi hiyo inalenga kukuza vipaji vya wasanii wa ndani kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo programu ya Rangi Nyumbani Residency inayowaunganisha wabunifu wa Kitanzania na mitandao ya kimataifa.