Nyota wa Bongo Fleva, Billnass amesema mapenzi yake kwa mkewe Nandy yaheshimiwe huku akiwachana wanaomfuatilia kwa mabaya katika ndoa yao.
Billnass anasema watu wengi wamekuwa wakidhani uhusiano wake na Nandy ni kwa sababu ya pesa za mwanadada huyo anayefanya vizuri katika Bongo Fleva na si mapenzi na hapa ameamua kuweka wazi kila kitu ikiwamo tetesi za kuachana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Billnass anasema kuhusu ndoa yao inawaumiza wengi na wanatamani waachane na ndiyo maana wanaleta maneno mengi, lakini anachojua wao wako vizuri na hazuii watu kuongea.
Billnass anayetamba na nyimbo nyingi kama Boda, Magetoni, Maokoto, Chafu Pozi, Ligi Ndogo na nyingine nyingi aliiambia safu hii midomo ya watu siku zote haiishi kusema na wanatumia mitandao kujazana uwongo jambo ambalo hajali.
"Hivi kwa nini watu hupenda kusema nimefata pesa kwa Nandy? Yaani wananichukuliaje? Ujue huwa nawashangaa sana watu hao, halafu nifuate pesa kwa Nandy kwani amekuwa benki? Halafu watu hao wanaosema hivyo ni wazi watakuwa masikini sana kwa sababu sijawahi ona Nandy kama ana pesa sana, wao sasa wanaomuona ana pesa maana yao wana hali ya chini."
Chanzo: Mwananchi Scoop