Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Dkt.Kemdon Mapana ametangaza rasmi kuwa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) zitatolewa Disemba 13, 2025 ambapo tuzo 36 zitatolewa katika vipengele mbalimbali.
Dkt. Mapana ameyasema hayo hii leo Oktoba 24, 2025 katika Ofisi za BASATA Posta Jijini Dar es Salaam na amesisitiza kuwa maandalizi ya Tuzo yanaendelea vizuri na kwamba dirisha la wasanii kuwasilisha maombi yao limefunguliwa rasmi kuanzia leo ambapo vipengele 36 vya tuzo vitatolewa mwaka huu.
“Tuzo zetu za Muziki Tanzania zitafanyika tarehe 13 Desemba 2025. Baada ya uchaguzi kumalizika, tutakuwa na tukio hili kubwa la kitaifa na dirisha la wasanii kuomba kushiriki limefunguliwa kuanzia leo na kila msanii aombe katika kipengele kinachomhusu.” amesema Dkt. Mapana.
Aidha Dkt. Mapana amewataka wasanii wote wanaotaka kushiriki kuanza kujisajili mapema na kuhakikisha wanawasilisha nyimbo za mwaka 2024 ambazo zina maadili mazuri na ujumbe chanya kwa jamii.
Chanzo: Millard Ayo