Dada yake mwanamuziki Dolly Parton amewaomba mashabiki kumuombea mwimbaji huyo wa Marekani, kutokana na matatizo ya kiafya ambayo hayajabainishwa.
Gwiji huyo wa muziki wa Country mwenye umri wa miaka 79 aliahirisha matamasha ya Disemba, akiwaambia mashabiki anahitaji "taratibu za kitabibu" ili kukabiliana na "changamoto za kiafya" zinazoendelea.
"Jana usiku, nilikuwa nimekesha usiku kucha nikimuombea dada yangu, Dolly," Freida Parton aliandika kwenye Facebook. "Wengi wenu mnajua hajisikii vizuri hivi karibuni." "Kwa kweli ninaamini katika nguvu ya maombi, na nimeongozwa kuuomba ulimwengu wote unaompenda kuwa mashujaa wa maombi na kuomba pamoja nami." Freida alimalizia ujumbe wake.
"Ana nguvu, anapendwa, na maombi yote yakiinuliwa kwa ajili yake, najua moyoni mwangu atakuwa sawa," aliandika. "Godspeed, sissy yangu Dolly. Sote tunakupenda!"
Parton alikuwa ameratibiwa kufanya maonesho sita katika The Colosseum katika Caesars Palace mwezi Desemba.
Lakini aliahirisha maonesho hayo hadi Septemba mwaka ujao, akieleza kuwa hatakuwa na muda wa kutosha wa kuyafanyia mazoezi.
Parton hakufichua asili ya masuala ya afya yake, lakini hivi karibuni alilazimika kujiondoa kwenye hafla ya Dollywood baada ya kugunduliwa na jiwe la figo ambalo alisema lilikuwa linasababisha "matatizo mengi".
Mapema mwaka huu, alipoteza mume wake mpendwa Carl Dean baada ya karibu miaka 60 ya ndoa.
Baadaye alitoa wimbo mpya, If You Had Been There, kwa kumbukumbu yake.
Mwanamuziki huyo anafahamika zaidi kwa vibao vingi vya country crossover vikiwemo Coat of Many Colours, I Will Always Love You, 9 To 5 na Jolene.
Chanzo; Bbc