Viongozi wa biashara na maafisa wa serikali wametaka kasi ya utekelezaji wa mageuzi ya uwekezaji kuongezeka, mazingira ya biashara kuboreshwa, na miradi ya miundombinu ya kimkakati kuharakishwa, huku Tanzania ikiendelea kusukuma malengo ya Dira 2050.
Wito huo ulitolewa katika Mkutano wa Majadiliano ya Kila Mwezi ulioandaliwa na JUkwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEO Roundtable of Tanzania -CEOrt) jijini Dar es Salaam, uliowakutanisha maafisa wa serikali, viongozi wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo kujadili masuala yanayoathiri uchumi wa Tanzania na njia za kufungua fursa za uwekezaji nchini.
Mkutano huo, uliofadhiliwa na Heritage Insurance, ulifanyika katika Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro, ukiwa na kaulimbiu isemayo *“From Policy to Implementation: Unlocking Tanzania’s Investment Opportunity.”*
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Bw. Gilead Teri alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kujijengea nafasi kama kituo cha uwekezaji kinachoshindana kikanda kupitia maendeleo ya miundombinu, mageuzi ya sheria na uwekezaji katika rasilimali watu.
Alitaja sekta kama nishati, sayansi na teknolojia, usafirishaji wa pamoja (integrated logistics), mageuzi ya kidijitali, utafiti na maendeleo kama nguzo muhimu za kufanikisha Dira 2050, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.
Aidha, alibainisha kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Blueprint ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sekta ya madini na uchimbaji ilikuwa miongoni mwa zinazoongoza mwaka 2024, huku sekta nyingine pia zikionyesha mchango mkubwa katika kukuza uchumi.
“Hakika kuna dhamira ya makusudi kwa sasa kuelekea kufanikisha malengo ya Dira 2050,” alisema.
Alitaja miradi kama uboreshaji wa reli, upanuzi wa bandari na maendeleo ya sekta ya usafirishaji kama ishara ya kasi ya uwekezaji nchini.
“Ukizungumza na wadau wa usafirishaji na logistics, ongezeko la mizigo inayopita ni uthibitisho kuwa Tanzania inawekeza katika kasi na ufanisi,” alisema.
Aliongeza kuwa uwekezaji endelevu wa serikali katika miundombinu ni muhimu katika kurahisisha biashara na kuhakikisha bidhaa zinawafikia wananchi na masoko ya ndani na nje kwa urahisi.
Pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi kupitia mageuzi ya kisera na kisheria yanayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Kwa mujibu wake, mageuzi yaliyofanyika katika miaka ya hivi karibuni, yakiwemo mabadiliko ya sheria za uwekezaji na kuanzishwa kwa taasisi mpya za uwekezaji, yanasaidia kujenga mazingira rafiki zaidi ya biashara.
“Tumeweza kupiga hatua kubwa kwa miaka iliyopita, ingawa wakati mwingine maendeleo hayaonekani kwa haraka,” alisema.
Mwenyekiti wa CEOrt, David Tarimo, alisema sekta binafsi iko tayari kusaidia ajenda ya mageuzi ya kiuchumi ya muda mrefu ya nchi, lakini akasisitiza umuhimu wa uthabiti wa sera na mifumo madhubuti ya utekelezaji.
“Ufanisi wa Dira 2050 hautategemea tu sera nzuri bali pia jinsi tunavyoweza kuweka mazingira wezeshi kwa biashara kuwekeza, kubuni na kupanuka,” alisema.
Alibainisha kuwa mazungumzo ya mara kwa mara kati ya sekta ya umma na binafsi ni muhimu katika kutafuta suluhisho la vitendo na kuimarisha ushirikiano kuelekea malengo ya pamoja ya maendeleo.
Mjadala huo unakuja muda mfupi baada ya bajeti ya taifa kuwasilishwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo, ambapo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuendeleza viwanda, kuongeza mauzo ya nje na kukuza uchumi wa muda mrefu chini ya Dira 2050