Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ambaye alienguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), amesema bado anaendelea kufuatilia rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kuondolewa kwenye orodha ya wagombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza leo Oktoba 24, 2025, mara baada ya kufika katika Mahakama ya Rufaa Tanzania jijini Dodoma, Mpina amesema ziara yake ilikuwa ni ya kujiridhisha kama nyaraka za rufaa walizowasilisha kwa njia ya mtandao zimepokelewa rasmi na mahakama hiyo.
“Leo nimekuja kujiridhisha kama rufaa yetu tuliyowasilisha mtandaoni imepokelewa, na nimehakikisha kuwa kweli nyaraka hizo zimepokelewa rasmi na Mahakama ya Rufaa,” amesema Mpina.
Amesema baada ya kuthibitisha hilo, sasa anasubiri mahakama kupanga tarehe ya kusikiliza shauri hilo, ambalo linahusu kupinga hatua ya INEC kumuondoa kwenye orodha ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Tunasubiri sasa Mahakama ya Rufaa itupangie tarehe ya kusikilizwa kwa kesi yetu. Tuna imani na mhimili wa mahakama na tupo tayari kuendelea na hatua zote za kisheria,” ameongeza.
Mpina amewasilisha rufaa hiyo mapema mwezi huu akipinga uamuzi wa INEC wa kufuta jina lake katika orodha ya wagombea urais, akidai kuwa mchakato huo haukufuata taratibu za kikatiba na haki ya mtu kugombea nafasi za kisiasa nchini
Chanzo: Nipashe