Watanzania wamehamasishwa kutumia fursa ya kujisajili kwenye programu ya mawasiliano ya ujumbe iitwayo MAX, iliyotengenezwa nchini Urusi na ambayo imeanza kupata umaarufu miongoni mwa Warusi wanaoishi na kufanya kazi nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Boniface Assenga kutoka Russian House alisema kuwa MAX ni jukwaa la kipekee linalowawezesha watumiaji kuwasiliana kwa maandishi, kupiga simu za sauti na video, pamoja na kutuma faili bila vikwazo.
“MAX inaunganisha huduma zote muhimu zinazopatikana katika programu nyingine za mawasiliano ndani ya jukwaa moja, hivyo kurahisisha mawasiliano kwa watumiaji,” alisema Assenga.
Kwa sasa, programu hiyo ina zaidi ya watumiaji milioni 110 waliosajiliwa duniani, ambapo takribani milioni 7 wanaishi nje ya Urusi. Aidha, zaidi ya watumiaji milioni 80 hutumia programu hiyo kila siku wakinufaika na huduma mbalimbali ikiwemo simu za sauti na video, vituo vya taarifa (channels), simu za vikundi, kushiriki skrini na zana za mikutano ya mtandaoni.
Kwa mujibu wa watengenezaji wake, MAX inapatikana katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Asia, Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika Kusini. Mchakato wa kujisajili umetajwa kuwa rahisi, ambapo mtumiaji anahitajika kupakua programu, kuchagua nchi, kuingiza namba ya simu na kuthibitisha kwa msimbo wa SMS.
Assenga alisisitiza kuwa matumizi ya MAX hayalengi tu wanafunzi au wanaojifunza lugha ya Kirusi, bali mtu yeyote anayehitaji mawasiliano ya moja kwa moja na Warusi kupitia majukwaa ya taarifa na mawasiliano.
Kwa sasa, programu hiyo tayari imeanza kutumika katika nchi za Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Gambia, huku mipango ikiwa imekamilika kuisambaza zaidi katika nchi za Misri, Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Algeria na Tunisia.