Wadau Simanjiro waiomba Serikali kuyatambua rasmi madini ya Green Garnet kama miongoni mwa madini yenye thamani kubwa, kufuatia ongezeko la mahitaji ya madini hayo katika soko la kimataifa kutokana na uwepo wake kwa wingi katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Ushauri huo ulitolewa katika Mikoa ya Arusha na Manyara kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa madini vito, waongezaji thamani , wachimbaji na wamiliki wa leseni za uchimbaji , wakieleza kuwa madini ya Green Garnet (Tsavorite) yana thamani kubwa duniani lakini bado hayajapewa uzito unaostahili katika mifumo ya kisheria na kibiashara nchini.
Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Tanzanite mkoani Manyara Money Kassanga alisema, kutokana na kutokuwapo kwa tathmini rasmi ya thamani ya madini hayo , wengi wao huuza mawe hayo kwa bei ya chini isiyoakisi thamani halisi ya soko la kimataifa jambo linalopelekea kushusha thamani ya madini haya kuanzia kwa mchimbaji mpaka mfanyabiashara.
Kassanga aliongeza kuwa , kuwepo kwa hali hiyo imekuwa ikiwakosesha mapato stahiki na kupunguza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
“Mara nyingi tunachimba bila kujua thamani kamili ya mawe tunayopata. Kukosekana kwa taarifa rasmi za kimfumo na miongozo ndani ya nchi kunasababisha madalali kununua madini kwa bei ndogo sana kutoka kwa mchimbaji,” alisema Kassanga
Kwa upande wake mfanyabiashara wa madini ya vito mkoani Arusha, Peter Pereira alieleza kuwa, Tanzania ina madini ya vito aina mbalimbali yakiwemo madini green garnet (Tsavorite) ambayo kwasasa yanatambulika kama moja ya madini yenye thamani kubwa katika soko la kimataifa, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini waweke mikakati shirikishi itakayotambua na kuyaweka madini haya katika taswira ya kipekee.
Chanzo; Nipashe